LHRC HQ: Justice Lugakingira House
+255 22 2773038 / +255 22 2773048

MUHTASARI WA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA 2018/2019

  • MUHTASARI WA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA 2018/2019

MUHTASARI WA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA 2018/2019


Organization Report

Report attachment

Download

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) huandaa ripoti kuhusu biashara na haki za binadamu tangu mwaka 2012. Hivyo, hii ni ripoti ya sita kutengenezwa, ikiangazia namna makampuni na taasisi zingine zinavyozingatia sheria na viwango vya kazi, wajibu wa makampuni kuheshimu haki za binadamu, wajibu wa Serikali kulinda haki za binadamu na upatikanaji wa nafuu pale ambapo haki za binadamu katika sekta ya biashara zimevunjwa. Ripoti hii imejikita upande wa Tanzania Bara pekee.

Taarifa zilizopo katika ripoti hii zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo ufatifi uliofanyika katika mikoa 15 ya Tanzania Bara, ambapo makampuni 151 yalifikiwa, vikiwemo viwanda vidogo na vya kati. Jumla ya washiriki 2,118 walifikiwa na utafiti huu, ambao ni: wanajamii; maafisa na viongozi wa makampuni; wafanyakazi; maafisa wa mamlaka za usimamizi na udhibiti kwenye sekta ya biashara; maafisa wa vyama vya wafanyakazi; wafanyabiashara wanawake masokoni; watumiaji wa hudumaya usafiri; na maafisa kutoka halmashauri za wilaya. Taarifa pia zilipatikana kupitia ripoti mbalimbali za taasisi za Serikali, asasi za kiraia pamoja na vyombo vya habari. Mikoa iliyofikiwa ni: Dodoma, Dar es Salaam, Geita, Iringa, Mara, Mbeya, Songwe, Kimanjaro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Pwani, Shinyanga, Tanga, na Arusha.

Lengo kubwa la ripoti hii ni kuelezea hali ya biashara na haki za binadamu katika mwaka wa fedha 2018/ 19 kwa upande wa Tanzania Bara, ikionesha ni kwa namna gani makampuni yaliweza kuzingatia sheria za kazi, ardhi na mazingira; na namna gani makampuni hayo yaliheshimu au kuvunja haki za binadamu. Ripoti hii itatumika kama nyenzo ya kuboresha haki za binadamu katika sekta ya biashara nchini.

Muundo wa Ripoti

Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara 2018/ 19 ina jumla ya sura tisa. Sura ya Kwanza inaelezea kwa kifupi kuhusu Tanzania, biashara na haki za binadamu na uandaaji wa ripoti. Sura ya Pili inahusu uzingatiaji wa sheria na viwango vya kazi katika sekta ya biashara, ikijikita zaidi kwenye makampuni; huku Sura ya Tatu inaangalia utwaaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji, ikiangazia zaidi masuala ya fidia na uelewa kuhusu haki za ardhi. Sura ya Nne inahusu ulipaji kodi wa makampuni katika sekta ya biashara. Sura ya Tano inaangalia uwajibikaji wa makampuni kwa jamii na jukumu la makampuni kuheshimu haki za binadamu. Sura ya Sita imejikita katika ubaguzi wa kijinsia na aina nyingine za ubaguzi katika sekta ya biashara, huku Sura ya Saba ikiangalia utendaji na ufanisi wa mamlaka za usimamizi na udhibiti katika sekta ya biashara. Sura ya Nane inaangazia mazingira ya biashara na ulinzi wa walaji wa bidhaa, na mwisho kabisa Sura ya Tisa inatoa majumuisho na mapendekezo.